Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, amewasilisha Taarifa ya Randama ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU)

Katika uwasilishaji huo, Mhe. Ayoub amewasilisha taarifa ya Wizara pamoja na Vyombo vya Usalama vilivyo chini ya Wizara hiyo, vikiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), akieleza utekelezaji wa majukumu na mwelekeo wa bajeti kwa mwaka ujao wa fedha.
Aidha, amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa maoni na ushauri wa Kamati ya NUU, ambayo iliishauri Wizara kuweka utaratibu mzuri na unaotekelezeka wa kusimamia miradi ya maendeleo ili kuwezesha kuomba na kupata fedha za maendeleo kutoka Hazina kwa wakati kwa mafungu yote matano kwa kuzingatia mipango iliyowekwa.
Akifafanua kuhusu utekelezaji wa maoni hayo, Mhe. Ayoub ameeleza kuwa Wizara imeweka utaratibu mzuri na unaotekelezeka wa miradi ya maendeleo ili kuweza kuomba fedha za maendeleo Hazina kwa Vyombo vyake vya Usalama
Vilevile, hatua hizo zimewezesha upatikanaji wa shilingi bilioni 473.4 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, sawa na asilimia 114 ya shilingi bilioni 415.1 zilizotengwa katika bajeti ya maendeleo kwa Wizara pamoja na mafungu yake. Ambapo kiasi hicho kinajumuisha fedha zilizotolewa kutoka kwenye bajeti kuu ya Serikali kwa utekelezaji wa shughuli maalum kwa mwaka 2025/2026
Aidha, baada ya kupitia na kujadili taarifa hiyo, Kamati imeridhia kwa pamoja Mpango na Mapendekezo ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kwa mafungu yote matano.
Uwasilishaji huo umefanyika katika Ukumbi wa Kamati uliopo katika majengo ya Bunge jijini Dodoma leo Machi 26, 2026

