MAFUNZO YA COPRA YAWANOA MAAFISA UGANI 75 MOROGORO

Afisa Kilimo wa Halmashauri hiyo, Bw. Chesco C. Lwaduka,
English

Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imeendesha mafunzo maalum kwa Maafisa Ugani kata 75 wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha sekta ya kilimo kama mhimili mkuu wa uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Mvuha, yakilenga kuwajengea uwezo maafisa hao katika kusimamia miongozo ya uzalishaji endelevu wa mazao ya kimkakati hususan ufuta na mbaazi.
 

Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, Afisa Kilimo wa Halmashauri hiyo, Bw. Chesco C. Lwaduka, amesema wilaya imejipanga kuendeleza kilimo cha biashara chenye tija, huku mazao ya kipaumbele yakiwa ni ufuta na mbaazi, pamoja na mazao ya chakula kama mahindi, maharage na viazi.



Amesema mafanikio ya mazao hayo yanategemea kwa kiasi kikubwa juhudi za Maafisa Ugani, ambao ni kiungo muhimu kati ya sera za Serikali na utekelezaji wake kwa wakulima mmoja mmoja.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika msimu wa 2025/2026, COPRA imetoa jumla ya kilo 3,500 za mbegu bora kwa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro, ambapo kilo 568 ziligawiwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro. Mbegu hizo tayari zimepandwa na zinaendelea vizuri mashambani, huku zikitarajiwa kuongeza uzalishaji na kipato kwa wakulima.


 

Aidha, COPRA kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), imefanikisha upatikanaji wa masoko kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala na minada ya kidigitali.

Kupitia mfumo huo, katika msimu wa 2024/2025, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro iliuza kilo 4,850,396 za ufuta na kilo 5,288,212 za mbaazi. Mafanikio hayo yameongeza hamasa kwa wakulima wengi kuendelea kulima mazao hayo, hasa katika msimu huu ambao hali ya mvua imekuwa nzuri.

Katika mafunzo hayo, Maafisa Ugani wametakiwa kuandaa na kutekeleza mipango madhubuti ya utoaji huduma za ugani, kuhamasisha ushiriki wa vijana na wanawake katika uzalishaji, pamoja na kuhakikisha sehemu ya mapato yatokanayo na ushuru wa mazao (crop cess) yanaelekezwa katika kuendeleza sekta ya kilimo.

Mafunzo hayo yanatajwa kuwa chachu ya kuongeza tija, uzalishaji na mapato kwa wakulima wa Wilaya ya Morogoro, huku yakichochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo na taifa kwa ujumla.

 

Simplenews subscription

The subscriber's email address.
Stay informed - subscribe to our newsletter.