TAKUKURU YANUSURU MAMILIONI YA FEDHA ZA UMMA

Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Geita, Alex Mpemba
English

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Geita imefanikiwa kuzuia upotevu wa zaidi ya Sh milioni 94.21 zilizokuwa zimefujwa kupitia miradi ya maendeleo na malipo haramu.

Akizungumza na waandishi wa habari kuelezea utendaji wa taasisi hiyo kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka (Oktoba hadi Desemba 2026), Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Geita, Alex Mpemba, ameanika madudu yaliyokuwa yakifanyika kwenye miradi ya maendeleo na mifumo ya bima ya afya.

Moja ya mafanikio makubwa yaliyotajwa ni kurejeshwa kwa kiasi cha Shilingi milioni 32 zilizokuwa zimeidhinishwa kimakosa kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Mpemba amefafanua kuwa fedha hizo zilikuwa zikitumika kumpatia matibabu mtu asiyestahili baada ya mtuhumiwa mmoja (jina limehifadhiwa) kumuingiza mnufaika hewa kwenye mfumo huo kinyume cha sheria.

Vilevile, TAKUKURU imefanikiwa kurejesha Shilingi milioni 20 kwenye akaunti ya AMCOS IDOSELOMWALO. Fedha hizi ni sehemu ya mkopo mkubwa wa Shilingi milioni 245 uliotolewa na benki ya CRDB, ambapo usimamizi mbovu ulipelekea kusuasua kwa marejesho hayo mpaka taasisi hiyo ilipoingilia kati.

Katika hatua nyingine, uchunguzi wa TAKUKURU umebaini ujanja uliokuwa ukifanywa na wakusanya mapato wa halmashauri kwa kutumia mashine za kielektroniki za POS. Badala ya kuwasilisha fedha benki, baadhi ya watumishi wasio waaminifu walikuwa wakizifuja.

Kufuatia msako huo, kiasi cha Shilingi milioni 8.14 kimepelekwa kwenye akaunti ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita, huku Shilingi 154,100 zikipelekwa Nyang’hwale.

Aidha, Halmashauri ya Chato imepata jumla ya Shilingi milioni 5.6 (kutoka TANROADS na RUWASA) kama kodi ya huduma (Service Levy) ambayo ilikuwa haijawasilishwa ipasavyo.

Katika barabara ya Nzera-Nkome, mkandarasi alijaribu kufanya ujanja kwa kutumia kifusi cha mfinyanzi badala ya moramu iliyopo kwenye mkataba (BoQ). TAKUKURU ilizuia malipo ya Shilingi milioni 25.2 mpaka mkandarasi huyo alipolazimika kurudia kazi hiyo kwa viwango vinavyotakiwa.

Hali kadhalika, kiasi cha Shilingi milioni 300 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa kompyuta katika Kituo cha Afya Nyabirezi-Chato kimeokolewa. Hatua hii ilikuja baada ya kubainika kuwa kompyuta hizo hazikuwasilishwa kama ilivyopangwa, jambo lililopelekea fedha hizo kurejeshwa ili zitumike kama ilivyokusudiwa.

 

Simplenews subscription

The subscriber's email address.
Stay informed - subscribe to our newsletter.