Kutokana na ongezeko la mahitaji ya Umeme katika Mikoa ya Lindi na Mtwara, Shirika la Umeme tanzania (TANESCO) Mkoa wa Lindi limeanzisha mradi wa kuongeza uwezo wa kituo cha kupooza umeme cha maumbika kwa kufunga transfoma yenye uwezo wa zaidi ya megawati 15 kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 702.

Akizungumza wakati wa Ziara ya ukaguzi wa miundombinu hiyo iliyofanywa na kamati ya siasa Wilaya ya Lindi iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Victoria Mwanziva , Meneja wa Tanesco Mkoa wa Lindi, Mhandisi Teodory Hall, amesema mradi huo unalenga kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika, kupunguza msongamano wa mzigo katika miundombinu iliyokuwepo na kuimarisha huduma kwa wateja. ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 99.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Lindi Victoria Mwanziva amepongeza juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kuboresha huduma ya umeme wa uhakika kwa Wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Lindi wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu hiyo, wakieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaleta manufaa makubwa kwa Mkoa na Taifa kwa ujumla
