Rais Samia Suluhu Hassan amepokea Ripoti ya Tume ya Rais ya kutathmini maboresho ya mfumo wa Kodi Nchini huku akiagiza kuwepo kwa kodi ya haki na usawa kwa Wananchi pamoja na kuwa na tafsiri moja ya sheria ya kodi kati ya Mfanyabiashara na Afisa wa Kodi.
Tume hiyo iliundwa na Rais Dkt.Samia Julai 2024 ili kufanya tathimini ya kina ya Mfumo wa Kodi, kufuatia malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa Wawekezaji, na Wafanyabiashara kuhusu changamoto ya mifumo ya kodi Nchini.
Hafla hiyo imehudhuliwa na Viongozi mbalimbali Serikali na Vyama vya Siasa akiwemo Makamo wa Rais Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi, Rais wa Zanzibar na Mwenyeki wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ally Mwinyi na Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba.
Akizungumza mara baada ya kupokea Ripoti hiyo Rais Dkt.Samia anasema Serikali itachambua mapendekezo hayo kwa kina na kuyafanyia kazi kwani maboresho ya mifumo ya kodi ni nyenzo muhimu ya kufikia lengo la Dira ya Taifa 2050.
Rais Dkt Samia anasema Ripoti hiyo inatarajiwa kutekelezwa kwa Vipindi tofauti kwani kutakuwa na utekelezaji wa muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu huku akikisisitiza kuwa anatamani itekelezwe kabla ya muda wake wa Urais kuisha 2030.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume hiyo Balozi Ombeni Sefue anasema Tume imependekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Kodi, Kutunga sheria na sera ya Taifa ya Kodi Nchini pamoja na kubadilishwa kwa mtazamo wa utendaji kazi wa Mamlaka ya mapato Tanzania.

Ripoti hiyo imeeleza hatua kadhaa ikiwemo kurahisisha mifumo ya kodi, kupunguza baadhi ya tozo zisizo za lazima pamoja kuongeza teknolojia katika ukusanyaji wa mapato.


