Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Miundombinu, Ardhi na TEHAMA imeeleza kuridhishwa na maendeleo ya miradi ya ujenzi na maboresho ya miundombinu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA), ikisema miradi hiyo inakidhi viwango vya kimataifa na itachangia kwa kiasi kikubwa kukuza sekta ya usafiri wa anga na uchumi wa Zanzibar.

Ziara hiyo imefanyika leo Jumanne, Machi 31, 2026, ambapo kamati ilikagua majengo ya Terminal 1, Terminal 2 na kituo cha biashara kilichopo ndani ya uwanja.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA), Seif Abdalla Juma, ndiye aliyewaongoza wajumbe wa kamati katika maeneo yote ya miradi, akiwapa maelezo ya kina kuhusu maendeleo yaliyofikiwa na mipango ya kukamilisha kazi zilizobaki.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati, Mh. Mihayo Juma Nunga amesema: “Kamati imefarijika sana na maendeleo ya miundombinu hii. Uwanja huu sasa unafanana na hadhi ya kimataifa. Tunatambua jitihada kubwa za ZAA chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu Seif Abdalla Juma.”
Ameongeza kuwa maboresho hayo yatawapa nguvu mawakala wa ndege kuongeza juhudi za kuvutia mashirika mapya ya ndege.

“Ubora wa miundombinu uliopo unatoa fursa kubwa kwa mawakala wetu kutafuta mashirika mapya ya ndege yatakayokuja kuwekeza hapa Zanzibar”. Alisema
Kamati pia imeipongeza ZAA kwa utekelezaji wa miradi hiyo, ikisema uwekaji wa mifumo bora ya uendeshaji utakuwa miongoni mwa mambo yatakayomfanya Mkurugenzi Mkuu Seif Abdalla Juma kukumbukwa.
Hata hivyo, kamati imeitaka Mamlaka kuweka utaratibu madhubuti wa kulipa fidia kwa wananchi ili kupatikana eneo la wazi kwa ajili ya upanuzi zaidi wa uwanja.
“Ni muhimu sasa Mamlaka ikaweka utaratibu mzuri wa kulipa fidia kwa wananchi ili kupatikana eneo la wazi kwa maendeleo ya baadaye,” alisema Mwenyekiti.
Aidha, kamati imesisitiza umuhimu wa usimamizi wa karibu wa mkandarasi ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

“Tunasubiri kuona mkandarasi anakamilisha kazi ndani ya muda uliopangwa ili mwanzoni mwa mwaka mpya wa fedha wa 2026-2027 operesheni zianze rasmi,” Aliongeza Mh. Nunga.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Ali Said Bakari, aliishukuru kamati kwa ziara yake na maelekezo waliyopewa.
“Tunawashukuru wajumbe wa kamati kwa ushauri wao. Wizara itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi hii ili ikamilike kwa wakati,” alisema Mhandisi Ali Said Bakari.
:“Ufunguzi wa jengo hili utafanyika kwa kuzingatia matakwa ya wapangaji ili kuhakikisha linaanza kutumika kwa ufanisi mara moja.”
Kamati hiyo imesema inasubiri kwa matarajio makubwa ufunguzi rasmi wa miradi hiyo, ambayo inatarajiwa kuimarisha sekta ya usafiri wa anga na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.


