Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Mhe. Rahma Kassim Ali ameeleza azma ya Serikali ni kumaliza migogoro ya ardhi ifikapo 2030 kupitia Mradi wa Mfumo wa Usimamizi na Usajili wa Ardhi (laris).

Akijibu hoja na masuala yaliyoulizwa na Wajumbe wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Miundo Mbinu, Ardhi na Tehama kwenye Semina ya Mafunzo kuhusu Majukumu ya Wizara ya Ardhi kwa Wajumbe, Mhe Rahma amesema Serikali iko mbioni kusaini Mkataba wa Mradi huo katika Siku za karibuni ili kuimarisha huduma za ardhi ikiwemo mipango miji na kumaliza Migogoro ya Ardhi.
Amesema kupitia Mfumo huo Wizara itajenga Ofisi kwenye Mikoa yote ya Zanzibar kwa lengo la kuwa karibu na Wananchi ili kutambua Maeneo yote na kuweka kumbukumbu sahihi za umiliki wa ardhi katika Maeneo hayo.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mihayo Juma Nunga ameshauri kuyafanyia kazi ipasavyo maoni yaliyotolewa na Wajumbe yanayohusu uimarishaji wa huduma za ardhi kwa vile yanagusa kwa kiasi kikubwa matakwa ya Wananchi.

Mapema Wakurugenzi wa Idara mbalimbali za Kamisheni ya Ardhi waliwasilisha Mada mbalimbali kuhusu majukumu ya Idara zao katika kutoa huduma za ardhi na utatuzi wa migogoro.



