Mkazi mmoja wa kata ya Mkata wilaya ya Handeni Mkoani Tanga Said Mbezi (23) amehukumiwa kifo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia ya kumlawiti mtoto wa miaka mitano.
Hukumu hiyo imetolewa Jumatano Januari 21,2026 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Pangani Fransisca Magwiza baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.
Awali ilielezwa mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo mnamo Oktoba 15,2024 katika kijiji cha Mkwaja wilaya ya Pangani kwa kumlawiti kijana wa miaka mitano ambae ni mwanafunzi wa darasa la awali.
Baadae lalamiko la tukio hilo riripotiwa kituo cha polisi Pangani siku hiyo hiyo na kesi ilifunguliwa na mtuhumiwa kuanza kutafutwa kwa tuhuma ya kumlawiti mwanafunzi huyo.

Septemba 16,2025 jeshi la polisi wilaya ya Pangani lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa na kukamilisha taratibu za upelelezi wa kesi hiyo na Septemba 18,2025 alifikishwa mahakamani kwaajili ya kusomewa shtaka.
Kesi hiyo ya kosa la kulawiti shauri lake lilisajiliwa Mahakamani CC NO.22726/2025 na ilipangwa kusikilizwa na hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Pangani Fransisca Magwiza.
Aidha awali baada ya mtuhumiwa kusomewa shitaka lake kwa mara ya kwanza Mahakamani alikana kutenda kosa hilo hivyo upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi mbele ya mahakama,mshtakiwa alikutwa na hatia ya kutenda kosa la Kulawiti na aliwasilisha utetezi wake ambao haukuwa na mashiko na ndipo mahakama ilimpatia adhabu ya kifungo cha maisha gerezani.
