BARAZA LA MADIWANI GEITA DC LASISITIZA UWAJIBIKAJI NA USHIRIKIANO KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI

MADIWANI GEITA
English

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Geita limefanya mkutano wake wa kawaida wa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026, huku likiweka msisitizo katika kuimarisha ushirikiano na uwajibikaji ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Mkutano huo uliofanyika leo Aprili 29, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri uliopo Nzera, ulihusisha mjadala wa kina wa taarifa za maendeleo kutoka katika kata zote 37. Taarifa hizo zimebainisha hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi pamoja na changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwakilishi wa Vyama Rafiki, Ndugu Ramadhan Sengerema, ameshauri baraza hilo kuhakikisha changamoto za miundombinu ya barabara zinatafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa mapato ya halmashauri na kuwarahisishia wananchi shughuli zao za kiuchumi.
Ndugu Sengerema amewahimiza madiwani kuendelea kufanya mikutano ya kisheria na wananchi ili kusikiliza kero zao, huku akisisitiza kufanya kazi kwa weledi na kushirikiana na wataalamu ili kuimarisha uaminifu kwa umma.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Geita, Komredi Michael Msuya, amelipongeza baraza hilo kwa utendaji kazi wake. Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuelekeza nguvu katika sekta ya elimu, hususan katika utatuzi wa kero ya madawati na ujenzi wa miundombinu ya vyoo mashuleni.

Aidha, Komredi Msuya ametoa wito kwa halmashauri kuendelea kushirikiana na sekta binafsi kupitia mifumo ya uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR), ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani humo.
Akifunga mkutano huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita.

Mhe. Jumanne Misungwi, amewataka madiwani kusimamia kikamilifu ukamilishaji wa miradi kwa wakati na kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unasimamiwa kwa uadilifu mkubwa.

Mhe. Misungwi amehitimisha kwa kusema kuwa ushirikiano wa dhati kati ya viongozi na wataalamu ndiyo msingi mkuu utakaowezesha halmashauri hiyo kufikia dhamira yake ya kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wa Geita.

 

Simplenews subscription

The subscriber's email address.
Stay informed - subscribe to our newsletter.